Thursday, March 11, 2010

Zenji washerehekea kurejea kwa umeme

Salma Said, Zanzibar

WANANCHI wa visiwa vya Zanzibar walikuwa ni wenye furaha baada ya umeme kurejea kwenye baadhi ya maeneo baada ya nishati hiyo kukosekana kwa miezi mitatu mfululizo.

Hata hivyo, pamoja na kutangazwa kwamba umeme ungeanza kupatikana saa 9:00 alasiri, nishati hiyo muhimu ilirejea saa 11:15 jioni huku lakini maeneo mengi bado hayajarejeshewa nishati hiyo ambayo kukosekana kwake kuliathiri kwa kiasi kikubwa hali ya uchumi wa Zanzibar.

Kaimu meneja wa Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), Ali Hassan Mbarouk aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kutokana na kukamilika kwa kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu kutoka nje ya nchi huduma ya umeme itarejea katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Meneja huyo pia aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuzima vyombo vinavyotumia umeme kwenye nyumba wanazoishi, akiwataka kuchomoa vifaa kama nyaya za jenereta kwenye mfumo wa umeme.

"Tunawaomba wananchi wote kufahamu kwamba huduma ya umeme itarejea sasa 9:00 kamili mchana na tunawaomba wananchi wote wachukue tahadhari kubwa kwa kuhakikisha kabla ya saa 9:00 wanazima 'main switch' zao pamoja na kuangalia katika tundu za umeme kama kumechomekwa misumari au vitu vya hatari kama hivyo ili kuepusha athari wakati umeme unaporejea," alisema meneja huyo.

Alisema kukosekana kwa umeme katika baadhi ya maeneo kunatokana na kuharibika kwa miundombinu kulikotokana na nyaya kuibiwa katika kipindi ambacho umeme ulikosekana.

"Pamoja na kurejea kwa huduma ya umeme, yapo baadhi ya maeneo ambayo umeme hautarejea kwa kuwa kuna baadhi ya sehemu nyaya zake zimechomolewa kwa hivyo tunawataarifu wananchi wa maeneo ambayo hawatapata huduma hiyo, wasisite kutoa taarifa kwa shirika letu na mafundi watakuja kurekebisha ili watu wote wapate huduma hiyo," alisema Mbarouk.

Maeneo ambayo hayajapata umeme ni pamoja na baadhi ya sehemu za Mji Mkongwe, Bububu, Kiembe Samaki, Mbweni, Mazizini na Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Meneja huyo alisema kazi ya matengenezo inaendelea vyema na muda sio mrefu wananchi wanaokosa huduma hiyo wataweza kupata umeme kama kawaida baada ya mafundi kuhakikisha wanafanya kazi hiyo usiku na mchana.

Hata hivyo, alisema serikali inawaomba radhi wananchi kutokana na tatizo hilo huku ikiwapongeza kwa kuonyesha uvumilivu katika kipindi chote cha miezi mitatu ya tatizo la umeme.

Watu walioongea na Mwananchi jana walionyesha furaha yao kutokana na kurejea kwa nishati hiyo muhimu ambayo iliathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya wakazi wa Zanzibar.

Pia wizi wa nyaya za umeme ulishamiri kwa kasi kubwa siku chache baada ya huduma ya umeme kuanz akukosekana Desemba 10 mwaka jana kutokana na hitilafu ya chombo cha kupokelea huduma hiyo kulipuka eneo la Fumba, mkoa wa Mjini Magharibi.

Kwa mujibu wa mafundi waliokuwa wakifanya matengenezo hayo kutoka Ras Kiromoni Dar es salaam hadi Fumba Mjini Unguja, kazi iliyofanyika ni kubwa na imegharimu mabilioni ya fedha kutokana na kununua vifaa vipya vya kupokelea umeme huo kutoka katika gridi ya taifa.

Hii ni mara ya pili kwa kifaa hicho kulipuka. Kililipuka kwa mara ya kwanza mwaka 2008 na umeme kukosekana kwa takriban mwezi mmoja.

No comments:

Post a Comment